Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa kauli ya kushangaza akimhusisha Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, na kuanzisha mzozo unaoendelea kati ya Ukraine na Urusi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Trump alisema kuwa kiongozi huyo wa Ukraine alifanya makosa kwa kuingia kwenye vita na taifa lenye nguvu kubwa kama Urusi, hasa bila kuwa na uhakika wa kushinda.
“Huwezi kupambana na taifa lililo mara kadhaa kubwa kuliko lako na kutegemea msaada wa silaha kutoka nje,” alisema Trump.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia mashambulizi makali ya Urusi katika mji wa Sumy nchini Ukraine, ambapo zaidi ya watu 30 walipoteza maisha katika tukio hilo linalotajwa kuwa baya zaidi kwa mwaka huu.

Trump hakusita kuwataja watu watatu anaowaona kama chanzo cha vita – akiwemo Rais Vladimir Putin wa Urusi, Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden, na Zelensky mwenyewe.
“Vifo vya watu wengi vimesababishwa na watu watatu: Putin, Biden ambaye hakuwa na mwelekeo, na Zelensky,” alisema.
Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa idadi ya waliouawa au kujeruhiwa ni mamia ya maelfu, kinyume na madai ya Trump ya kuwa “mamilioni” wamepoteza maisha.
Katika kauli nyingine, Trump alidai kuwa Zelensky amekuwa akiomba msaada wa makombora muda wote na kuhoji uwezo wake wa uongozi.
“Kabla ya kuanzisha vita, unapaswa kuhakikisha una uwezo wa kushinda,” aliongeza.
Wakati huo huo, Zelensky aliwahi kutoa mwito kwa Trump kuitembelea Ukraine kabla ya kuamua kufikia makubaliano yoyote ya kumaliza vita na Rais Putin.
Taarifa hii pia imeibua kumbukumbu ya mvutano uliowahi kutokea kati ya Trump na Zelensky katika mkutano wao wa Februari, ambapo hali ya kutokuelewana iliibuka wazi.


